Mandhari yapendeza, kwa hakika si utani,
Mazingira kukoleza, uzuri uso kifani,
Majengo kahanikiza, pia nzuri bustani,
Chuo Kikuu cha Chuka, Chuo kizuri hakika.
Katabiri Bi Kanyua, miaka ya hamsini,
Mlima utaja kua, maeneo ya Ndagani,
Na kweli yakatimia, chuo hiki yamkini,
Chuo Kikuu cha Chuka, Chuo kizuri hakika.
Naibu wa chansela, ustadhi Bwana Njoka,
Katujali masuala, yakaweza kututoka,
Hawezi katu kulala, tukiwa kwenye mashaka,
Chuo Kikuu cha Chuka, Chuo kizuri hakika.
Wenye heba wahadhiri, nzuri ya kutamanika,
Hawatokutia shari, ujuzi kajirundika,
Tumeweza kunawiri, maarifa katuweka,
Chuo Kikuu cha Chuka, Chuo kizuri hakika.
Za kila nui shahada, diploma uzamifu,
Zaidi stashahada, uzamili yake kufu,
Mashahada ya ziada, na digrii lufufu,
Chuo Kikuu cha Chuka, Chuo kizuri hakika.
Wanafunzi nawaita, chuo hiki kujiunga,
Elimu bora kupata, kesho yenu kuipanga,
Mfike bila kusita, mbele zaidi kusonga,
Chuo Kikuu cha Chuka, Chuo kizuri hakika
A.L.Maingi Ndungi.
"Malenga Mamboleo"
0 comments:
Post a Comment
Thanks for your comment on our blog!