pub-4564465823266615 'MASIPONSA' by Riziki Tokal ~ Writers Guild Chuka University

Monday, 22 October 2018

'MASIPONSA' by Riziki Tokal



Ninakuja kwa makeke, ujumbe wangu kusema,
Ili kwenu usikike, vijana watu wazima,
Hasa kwa wana wa kike, kutunza yetu heshima,
Si watu waone vile, masiponsa ni wanyama.

Imekuwa lalamiko, toka bara hadi pwani,
Vimesheheni vituko, masiponsa vileleni,
Chunga hao ni wanoko, hawakupendi yakini,
Si watu waone vile, masiponsa ni wanyama.

Ni wakwasi kwelikweli, pesa tele mifukoni,
Lakini ni makatili, pulika wangu mwendani,
Bura yako sibadili, kwa kutamani rehani,
Si watu waone vile, masiponsa ni wanyama,

Usifuate tamaa, ukasahau mauti,
Hawachoki kuhadaa, kwa huba za chokileti,
Wakikufwata kataa, sihadaike na noti,
Si watu waone vile, masiponsa ni wanyama.

Thamani kwao hauna, chunga hao ni mafisi,
Pindi wakishakuchuna, watatoweka kwa kasi,
Na katu hutawaona, imekwisha yenu kesi,
Si watu waone vile, masiponsa ni wanyama.

Acheni kujiumbua, kwa kuvitaka vya ghali,
Masiponsa wanaua, ina sumu yao mili,
Wahepeni nawambia, wanashinda Pilipili.
Si watu waone vile, masiponsa ni wanyama,

Mwisho hapa natuama, siwezi tena andika,
Ujumbe niliosema, ushikeni kwa haraka,
Musije uweke nyuma, moyoni kuufundika,

Si watu waone vile, masiponsa ni wanyama


Na Riziki Tokal

0 comments:

Post a Comment

Thanks for your comment on our blog!